Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Haki za Binadamu Kufanya Kikao Maalum Kuhusu Mauaji El-Houleh, Syria

Baraza la Haki za Binadamu Kufanya Kikao Maalum Kuhusu Mauaji El-Houleh, Syria

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa litafanya kikao maalum Ijumaa Juni 1, kuhusu hali ya haki za binadamu inayoendelea kuzorota nchini Syria na mauaji ya hivi karibuni ya El-Houleh. Kikao hicho kitakuwa cha 19 cha aina yake, na cha nne kuihusu Syria.

Ombi la kufanyika kikao maalum limewasilishwa katika barua hii leo na mabalozi wa Qatar, Uturuki, Marekani, Saudi Arabia, Kuwaiti, Denmark na Muungano wa Ulaya.

Ombi hilo lilitiwa saini na mataifa 21 wanachama wa baraza hilo, na mataifa 30 waangalizi. Ili kikao kama hicho kifanyike, ni lazima kipate uungwaji mkono na thuluthi moja ya uanachama wa baraza hilo- yaani mataifa 16 au zaidi yanahitajika kutia saini.

Baraza la Haki za Binadamu lilifanya kikao cha kwanza maalum kuhusu Syria mnamo Aprili 29 mwaka 2011, cha pili Agosti 22, 2011, na cha tatu Disemba 2 2011.