Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa Vyombo vya Sheria ni lazima Uimarishwe kama sehemu ya Demokrasia Pakistan:UM

Uhuru wa Vyombo vya Sheria ni lazima Uimarishwe kama sehemu ya Demokrasia Pakistan:UM

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa majaji na mawakili, Gabriela Knaul, ametoa wito kwa serikali ya Pakistan izishughulikie changamoto zilizosalia kuhusu uhuru wa vyombo vya sheria, licha ya kuelezea kuridhika kwake na maendeleo ya kidemokrasia yaliyofanywa nchini Pakistan miaka ya hivi karibuni.

Bi Knaul ameyasema haya wakati akikamilisha ziara yake rasmi nchini humo, kati ya tarehe 19 na 29 Mei 2012, ambayo ndiyo imekuwa ya kwanza kufanywa na mtaalam huru wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 13. Bi Knaul ameongeza kuwa, uhuru wa vyombo vya sheria unapaswa kuimarishwa ili taifa hilo lisipoteze ufanisi uliofikiwa katika kipindi cha mabadiliko ya kidemokrasia.

Ameelezea hofu yake kuwa, kuwepo kwa Mahakama mbili kuu katika katiba ya Pakistan- yaani Mahakama Kuu na Korti ya Shariat- kunaleta utata, kwani kunatoa nafasi ya kufanya ufafanuzi wenye kukanganya.

Pia, Bi Knaul ameelezea kusikitishwa kwake na idadi na aina ya kesi ambazo zimeripotiwa za vitisho na mashambulizi dhidi ya majaji na mawakili na kusema kuwa, usalama wa maafisa wa sheria ni muhimu, ili kuwawezesha kufanya kazi bila vizuizi au matatizo yoyote. Pia amesema kuwa ni lazima vyombo vya habari vipewe vifaa na rasilmali za kutosha ili utendaji kazi uwezekane. Wakati wa ziara yake pia amezingatia uhusishaji wa maswala ya jinsia na haki za wanawake katika ngazi zote za sheria.