Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanariadha washiriki katika kuadhimisha miaka 40 ya shirika la UNEP

Wanariadha washiriki katika kuadhimisha miaka 40 ya shirika la UNEP

Mamia ya wanariadha wameshiriki katika mbio za kuadhimisha miaka 40 tangu kuundwa kwa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP.

Zaidi ya wakimbiaji 200 wameshiriki katika mashindano ya mbio za nusu-marathon mjini Nairobi, ambao ndio makao makuu ya UNEP, huku wengine zaidi ya 300 wakitimua mbio za kilomita tano kujiridhisha wenyewe, UNEP imesema.

Washindani wengi katika nusu-marathon walikuwa ni wakimbiaji hodari waliotumia nafasi hiyo kujitayarisha kwa mashindano kama vile London Marathon Aprili, na pia Olimpiki ya mwaka huu ambayo pia itafanyika mjini London Agosti.Vigogo na maafisa kutoka nchi 150 waliohudhuria mkutano wa Baraza Kuu la UNEP walishiriki pamoja na mabingwa kama vile Patrick Makau, anayeshikilia rekodi ya ulimwengu ya marathon, na Paul Tergat, mkimbiaji hodari aliyewahi kushikilia rekodi hiyo mara kadhaa.

Bwana Tergat pia anahudumu kama balozi dhidi ya njaa katika shirika la Umoja wa Mataifa la chakula, WFP.