Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Maldives hatimaye akubali kujiuzulu

Rais wa Maldives hatimaye akubali kujiuzulu

Rais wa Maldives hatimaye amesalimu amri na kukubali kuachia madaraka ikiwa ni siku chache tu baada ya kuandamwa na mashinikizo yaliyomtaka kuondoka Ikulu. Rais Mohamed Nasheed amekuwa kwenye shinikizo kubwa toka kwa wale wanaopinga utawala wake na katika siku za hivi karibuni maandamano ya kumtaka atachia ngazi yalivuka mipaka na kuudhorotesha uongozi wake.

Amekubali kukabidhi madaraka kwa makamu wake. Nasheed ndiye rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia na wengi wanamtaja kama mtu aliyeweza kuhamasisha watu kuwa na utambuzi juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa taifa hilo.

Kufuatia hatua hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea matumaini yake akisema kuwa hatua ya kukabidhi madaraka kwa msaidizi wake itakuwa fursa njema kwa taifa hilo kujiepusha na vitendo vya umwagaji wa damu.