Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM aitaka Canada kuzingatia ustawi wa jamii ya Attawapiskat ambao ni asili ya nchi hiyo

Mtaalamu wa UM aitaka Canada kuzingatia ustawi wa jamii ya Attawapiskat ambao ni asili ya nchi hiyo

Mtaalamu huru anayefungamana na Umoja wa Mataifa katika eneo la haki za binadamu, ameitolea mwito Canada kuchukua hatua za haraka kuboresha hali ya ustawi wa baadhi ya wananchi wake ambao wanaendelea kuishi maisha ya taabu na dhiki huku wakikosa baadhi ya huduma muhimu ikiwemo maji.

James Anaya ambaye anahusika zaidi na ustawi wa wananchi wazawa amesema kuwa jamii ya watu wa Attawapiskati wanaishi kwenye mazingira yasiyoridhisha hivyo serikali ya Canada inapaswa kutafakari upya namna inavyowashughulikia watu hao na makundi mengine pia.

Attawapiskat ni jamii ya watu asilia katika nchi ya Canada ambao sasa wanapatikana katika maeneo ya mbali huko Kaskazini mwa Ontario. Ina jumla ya watu wanaokadiriwa kufikia 1,800.

Hata hivyo hali jumla ya ustawi wao bado ni ya kiwango cha chini mno huku pia wakikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ukosefu wa dhana za kujimudu wakati wa kipindi cha majira ya baridi.