Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sauti za wanawake lazima zisikike wakati wa kipindi cha mpito na mabadiliko:Manjoo

Sauti za wanawake lazima zisikike wakati wa kipindi cha mpito na mabadiliko:Manjoo

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake Rashida Manjoo amesema hivi karibuni dunia imeshuhudia ushiriki wa wanawake katika maandamano kwenye sehemu mbalimbali duniani hali ambayo inadhuhirisha nia ya wanawake hao kuchagiza mabadiliko katika jamii ikiwa ni pamoja na kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu kwa ujmla, na hasa haki za binadamu za wanawake.

Amesema wakati wa mabadiliko ya kisiasa unatoa fursa ya kipekee kuhakikisha kwamba wanawake wanashiriki sawa na wanaume katika maisha ya jamii na kwamba haki zao za kisheria na mifumo ya jamii ikiwemo kutokomeza mifumo yote ya ubaguzi na ukatili zinalindwa kisheria na kwa vitendo.

Bi Manjoo amesema wanawake wamesimama pamoja na wanaume mitaani, msitari wa mbele katika mapambano ya kuwa na maisha bora na pia wametoa msaada mkubwa kwa waandamanaji. Wanawake ni miongoni mwa watu wanaolipa gharama kubwa wakati wa kipindi cha mpito cha kisiasa ikiwemo kubaguliwa, kuonewa na kufanyiwa ukatili. Wanawake wamebakwa, wamepukuliwa miili yao, wametukanwa na hata kudhalishwa kimapenzi.

Manjoo amesema la muhimu kila juhudi zifanyike kuhakikisha kwamba haki za wanawake zinachagizwa na kulindwa na unakuwepo usawa wa kijinsia kwani wanawake wana haki ya kushiriki katika masuala ya jamii kwa uhuru bila vitisho vya ukatili, na sauti zao lazima zikizwe na kutiliwa maanani wakati wa kipindi cha mpito.