Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zajidhatiti kuchukua hatua kuzuia wizi wa dawa

Nchi zajidhatiti kuchukua hatua kuzuia wizi wa dawa

Mkutano wa ngazi ya juu umefanyika mjini Addis Ababa Ethiopia chini ya ufadhili wa mfuko wa kimataifa yaani Global Fund ambao unapambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria na Roll Back Malaria. Mkutano huo wa pili una lengo la kushirikiana kuchukua hatua za kuzuia wizi na usambazaji haramu wa dawa.

Mkutano huo umewaleta pamoja takribani washiriki 100 na umehitimishwa leo kwa mawaziri wanane wa afya na wadau wengine wa utekelezaji wa program za afya kutathimini na kuimarisha mipango ya kuzuia wizi wa dawa.

Global Fund na washirika wengine wa kimataifa wameafikiana kuunga mkono hatua hiyo, wakitambua kwamba kupunguza wizi wa dawa kunawezekana tu ambapo nchi zinazoekeleza hatua hizo zitaimarisha mikakati na hatua za usalama kuhakikisha dawa zinawasili salama bila kuibiwa.

Kwa mujibu wa muongozaji mkutano huo ambaye ni naibu mkurugenzi wa mkuu wa Global Fund Debrework Zewdie mktano huu ni muhimu sana kwa vita dhidi ya usamabaji na wizi wa dawa. Wizi wa dawa ni tatizo sugu katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea hususani wizi wa dawa ambazo labda ni za bure au za gharama nafuu kwenye sekta za umma, lakini zinauzwa kwa gharama kubwa kwenye soko huria au katika nchi jirani.

Na tatizo linaendelea kutokana na ukosefu wa fedha kukabiliana nalo na mifumo mibaya ya usambazaji dawa katika nchi nyingi masikini.