Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya Cyprus yampa Ban matumaini ya muafaka

Mazungumzo ya Cyprus yampa Ban matumaini ya muafaka

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amesema ana imani kubwa kwamba muafaka wa kudumu katika suala la Cyprus utafikiwa kufuatia hatua kubwa iliyopigwa katika siku mbili za mazungumzo baina ya Cyprus ya upande wa Ugiriki na ile ya upande wa Uturuki viongozi wa pande hizo walipokutana hapa New York.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Ban amesema kiongozi wa Cyprus ya Ugiriki Dimitris Christofias na yule wa upande wa Uturuki Dervis Eroglu wamepiga hatua inayotia matumaini makubwa ya kufikia azima yao ya kumaliza mvutano huu.

Amesema viongozi wote wawili wamemtia shime kwamba suluhisho la kudumu litapatikana. Viongozi hao wawili wamekutana na Katibu Mkuu nje ya New York tarehe 30 na 31 Oktoba, ukiwa ni mkutano wa nne na mkuu wa Umoja wa Mataifa kama sehemu ya kuchagiza mazungumzo hayo yenye lengo la kuunganisha visiwa hivyo vya Mediteraniani.