Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusiwasahau watu wa DPRK wanaokabiliwa na matatizo ya chakula:Amos

Tusiwasahau watu wa DPRK wanaokabiliwa na matatizo ya chakula:Amos

Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea DPRK haiwezi kulisha watu wake katika siku zijazo, kwa mujibu wa mkuu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Valarie Amos. Ameitaka dunia kuongeza misaada ya kibinadamu na sio kuwapa mgongo watu hao ambao takribani milioni sita sasa wanategemea msaada wa chakula.

Bi Amos amewaambia hayo waandishi wa habari baada ya ziara ya siku tano nchini DPRK na kuongeza kuwa taifa hilo linasalia kuwa na shida ya chakula huku mgao ukipunguzwa, uzalisha mdogo na watoto wengi wakidumaa. Suluhisho mpya linahitajika ili kumaliza shida hii kubwa ambayo haionekani kuwa na mwisho, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari Beijing mara baada ya kuondoka DPRK.

Bi Amos alitembelea hospitali mbili, nyumba ya watoto yatima, kiwanda cha biskuti, shamba la jumuiya, soko, ghala la dawa , na kituo cha umma cha usambazaji. Pia alikutana na maafisa wa serikali, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wahisani, wanadiplomasia, wahudumu wa afya na akina mama.

Alibaini kwamba hali ya maisha imezidi kuzorota tangu katikati ya miaka ya tisini na kumaanisha watu wengi wanaendelea kuteseka nchini DPRK.