Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taka zitokanazo na masuala ya tiba zinazidi kuwa tatizo:UM

Taka zitokanazo na masuala ya tiba zinazidi kuwa tatizo:UM

Taka zitokanazo na tiba zinatoa tishio na kuwa tatizo kubwa duniani likiweka hatarini afya ya wahudumu wa afya, wagonjwa wafanyakazi wengine na mtu yoyote anayekutana na taka hizi ambazo hutupwa na hospitali na vituo vingine vya afya. Hii ni kwa mujibu wa mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu ambaye pia ni mwakilishi maalumu wa haki za binadamu na taka za sumu Calin Georgescu ambaye ametoa ripoti leo akionya kwamba dunia haishughulikii vya kutosha matatizo yanayosababishwa na taka za tiba.

Asilimia 20 hadi 25 ya taka zote zitokanazo na masuala ya tiba zinachukuliwa kama ni za hatari na zinaweza kuleta athari kwa afya na mazingira kama hazitashughulikiwa na kutupwa katika mazingira yafaayo.

Taka hizo za tiba ni pamoja na taka za kuambukiza maradhi, taka za mabaki ya mwili na viungo, madawa na vifaa ambavyo muda wake wa kutumia umepita, vifaa vya kemikali na vifaa vyenye ncha kali au vifaa ambavyo havitumiki tena.

Mtaalamu huyo amesema tatizo linaongezeka haraka hasa katika nchi zinazoendelea ambako kiwango cha taka kinapanda haraka kwa sababu ya kukuwa kwa sekta ya afya na uwezo wa kuhifadhi taka hizo inavyostahili huenda haupo. Amesema vitu kama sindano na vifaa vyenye ncha vinaweza kuambukiza maradhi kama virusi vya hepatitis B, hepatitis C na HIV.