Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara sasa kufanyika kupitia simu ya mkononi Liberia:ITC

Biashara sasa kufanyika kupitia simu ya mkononi Liberia:ITC

Kituo cha biashara cha kimataifa ITC kwa ushirikiano na Angie Brooks International ABIC leo wamezindua mradi nchini Liberia ambao utaruhusu wafanyabiashara kununua na kuuza bidhaa kupitia simu za mkononi. Mradi huo unaoitwa “biashara mkononi T@H umetangazwa na Rais wa Liberia Bi Ellen Johnson Sieleaf kwenye hafla maalumu iliyofanyika mjini Lofa ambako mawaziri mbalimbali pia wamehudhuria akiwemo wa biashara, viwanda na kilimo na wa vijana na michezo.

Mradi huo wa T@H ingawa ni huduma ya simu lakini unafanana na biashara zingine za mitandao kama e-Bay au Alibaba ambayo inawaruhusu wachuuzi kuweka bidhaa zao wanazouza kwenye mtandao. ITC inasema kununua na kuuza bidhaa kupitia teknolojia hii kutasaidia biashara miongoni mwa wakulima wa vijijini, wanawake wachuuzi sokoni, wafanyabiashara wadogowadogo, wamiliki wa migahawa na wasafirishaji. Mradi huo umeanzishwa mahususi kwa ajili ya Liberia na umefadhiliwa na serikali ya Finland.