Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watangaza njaa Kusini mwa Somalia

UM watangaza njaa Kusini mwa Somalia

Umoja wa Mataifa umeyatangaza rasmi maeneo mawili ya Bakool Kusini na Lower Shabelle nchini Somalia kama yanayokumbwa na njaa . Umoja wa Mataifa unasema kuwa watu milioni 3.7 kote nchini karibu nusu ya watu wote nchini Somalia kwa sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula na wanahitaji misaada ya dharura.

Somalia imekuwa ikishuhudia ukame wa muda mrefu kwa miaka michache iliyopita huku mzozo unaoendelea ukitatiza juhudi za mashirika ya kutoa misada kuwafikishia misaada wanaoihitaji. Mratibu wa huduma za UM nchini Somalia Mark Bowden anasema kuwa utapiamlo umefikia viwango vya juu zaidi duniani hadi asilimia 50 kwenye sehemu zingine za Kusini mwa Somalia.

(SAUTI YA MARK BOWDEN)

Hali ya njaa huwa inatangazwa tu wakati viwango vya utapiamlo miongoni mwa watoto vinazidi asilimia 30 , wakati zaidi ya watu wawili kati ya watu 10,000 wanapokufa kila siku na wakati  hawawezi kupata chakula na mahitaji mengine. Bowden anasema kuwa dola milioni 300 zinahitajika kwa muda wa miezi miwili ijayo kuwasaidia wanaohitaji misaada zaidi.