Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji katika elimu umeongezeka Afrika:UNESCO

Uwekezaji katika elimu umeongezeka Afrika:UNESCO

Ripoti iliyochapishwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO inasema nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara zimeongeza uwekezaji na matumuzi ya masuala ya elimu kwa zaidi ya asilimia 6 kila mwaka katika muongo uliopita.

Hata hivyo ripoti inasema licha ya uwekezaji huo bado nchi nyingi ziko mbali kufikia lengo la kutoa elimu bure ya msingi kwa kila mtoto.

Ripoti hiyo iitwayo kugharamia elimu katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kukabili changamoto za kupanua wigo, usawa na hadhi inatoa takwimu za kina kuhusu ufadhili wa elimu katika nchi 45 za Afrika.

Pia ripoti hiyo inatoa takwimu za historia za kufuatilia uwekezaji wa masuala ya elimu tangu kumalizika kwa kongamano la kimataifa la elimu mwaka 2000.

Mkurugenzi mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema ripoti hii inaonyesha bayana jinsi gani nchi za Afrika na washirika wao zilivyojidhatiti kufikia lengo la elimu kwa wote, na inaonyesha juhudi zao zinazaa matunda, kwani watoto wengi wanaenda shule hivi sasa kuliko zamani, hali inayotia moyo na itawachagiza wahisani kulisaidia bara hilo ili kuziba mapengo yaliyosalia katika elimu.

Amesema kati ya mwaka 2000 na 2008 idadi ya watoto walioingia shule za msingi imeongezeka kwa asilimia 48 kutoka milioni 87 hadi milioni 129. Nchi 25 kati ya 26 zimeongeza bajeti ya elimu ikiwemo Burundi na Msumbiji.