Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu kujadili hali ya Syria

Baraza la haki za binadamu kujadili hali ya Syria

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa litafanya kikao maalumu kujadili hali ya Syria Ijumaa April 29.

Ombi la kufanyika kwa kikao hicho maalumu limetolewa na Marekani na kuungwa mkono na nchi wanachama 16 wengi wakiwa kutoka muungano wa Ulaya. Kikao hicho kitafanyika kukiwa na ongezeko la hofu kubwa juu ya msako unaoambatana na ghasia dhidi ya waandamanaji wanaopinga serikali, ambapo inadaiwa mamia ya watu wameuawa na vikosi vya serikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali ghasia hizo na kuitaka serikali ya Syria kukomesha umwagaji damu dhidi ya waandamanaji wanaotaka mabadiliko. Ban ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru dhidi ya mauaji hayo.

Kamishna wa haki za binadamu amesema watu zaidi ya 100 wameuawa katika miji mbalimbali ya Syria mwishoni mwa wiki na kusema hali hiyo haikubaliki.