Ban azungumza kwa simu na wadau wa demokrasia Niger

30 Machi 2011

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewapigia simu wahusika wakuu katika uchaguzi wa karibuni nchini Niger na kuwapongeza utu, uongozi na utaifa waliouonyesha katika kipindi cha mpito cha kuelekea demokrasia.

Februari mwaka jana wanajeshi waasi walivamia ikulu na kumtoa aliyekuwa Rais wakati huo Mamadou Tandja ambaye anashutumiwa na wapinzani na wengine kwa kukiuka demokrasia. Baraza la utawala wa kijeshi likavunja serikali na kusitisha katiba ambayo ingemruhusu bwana Tandja kusalia madarakani baada ya muda wake.

Ban amempigia Luteni jenerali Salou Djibo mkuu wa baraza kuu na kumpongeza kwa kurejesha demokrasia, amesema ameridhika na njia iliyotumiwa na Niger katika kipindi cha mpito na kupata katiba mpya. Pia amezungumza na Mahamadou Issoufou aliyetangazwa mshindi na tume ya uchaguzi ambaye anatarajiwa kuapishwa rasmi April 7 na pia Seini Oumarou aliyekubali kushindwa katika uchaguzi huo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter