Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa OCHA anatathimini hali DR Congo

Mkuu wa OCHA anatathimini hali DR Congo

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos yuko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika ziara ya siku mbili kutathimini mahitaji ya msaada.

Akiwa nchini humo Bi Amos atazuru majimbo mawili yaliyoathirika zaidi na vita , jimbo la Kivu Kaskazini lililoko Mashariki mwa nchi hiyo na jimbo la Orientale lililoko Kaskazini Mashariki. Bi amos amesema DR Congo haipati kipaumbele inachostahili. George Njogopa ana ripoti.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Akielezea hali jumla ya mambo kwenye eneo hilo, Mkuu huyo amesema kuwa mamilioni ya watu walioko kwenye maeneo ambayo yamekumbwa na machafuko bado wangali na kiu kubwa ya kupata amani na usalama na jambo la kustaajabisha zaidi ni kwamba bado wanakabiliwa na mkwamo wa ufikiwaji wa huduma za kibinadamu.

Jamhuri ya Congo inaandamwa na matatizo chungu nzima ambayo kila uchao huchukua sura nyingine kutokana na kuendelea kukua kwa matatizo ya kukosekana kwa huduma za usamaria mwema.

Hali ya umaskini, kuwepo kwa hali duni ya maendeleo na kushamiri kwa matukio ya ufunjifu wa haki za binadamu ni maeneo mengine ambayo yanaendeleza kuiandama nchi hiyo.

Hata hivyo Valerie Amos amesema kuwa amewasili nchini humo ili apate kujionea kwa macho yake namna hali ya mambo ilivyo ili hatimaye kusaka njia za haraka kwa kushirikiana na serikali kuzitanzua kasoro hizo.