Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yahofia afya na usalama wa watoto Libya

UNICEF yahofia afya na usalama wa watoto Libya

Watoto zaidi ya milioni 1.7 nchini Libya huenda wakakabiliwa na wakati mgumu mbele yao kutokana na mtafaruku wa kisiasa unaoendelea nchini humo limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Shirika hilo linasema linahofia hususani usalama , afya na viwango vya lishe kwa watoto karibu milioni moja Magharibi mwa Libya ambako fursa ya kuwafikia watu wanaohitaji msaada ni ndogo.

Akizungumza mjini Geneva naibu mkurugenzi mkuu wa UNICEF Hilde Jonhnson amesema ingawa matatizo ya kibinadamu hivi sasa kwenye mipaka ya Libya yanawaathiri zaidi watu wazima hususan wanaume wafanyakazi wahamiaji , hali inaweza kubadilika haraka kwa watoto na wanawake nchini humo.

(SAUTI YA HILDE JOHNSON)

Wakati huohuo UNICEF inaomba dola bilioni 1.4 ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu kwa watoto na familia zao kwenye nchi 32 duniani kwa mwaka huu 2011.