Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa ajira Gaza ni adha kubwa:UNRWA

Ukosefu wa ajira Gaza ni adha kubwa:UNRWA

Kupungua kwa kiwango cha mishahara na kuendelea kudhoofika kwa hali ya kibinadamu Gaza kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Israel kumesababisha adha kubwa na kuliweka eneo hilo katika hatihati ya kuporomoka kabisa.

Haya ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa Wapalestina UNRWA. Mwaka 2007 Israel iliweka vikwazo Gaza baada ya Hamas kushika udhibiti wa eneo hilo. Kwa mujibu wa Christopher Gunness, msemaji wa UNRWA tatizo la ajira Gaza ambalo sasa limefikia asilimia 45.5%, limewafanya watu wa eneo hilo kupoteza matumaini.

Ameongeza kuwa kubwa kabisa linalotia hofu ni kushuka kwa viwango vya mishahara. Kuanzia nusu ya kwanza ya 2009 hadi nusu ya kwanza ya 2010 mishahara ya kila mwezi ya watu imepungua kwa asilimia 9.5 hivyo kuwaongezea dhiki zaidi watu kwani hawana fedha mfukoni.

Mwaka jana Israel ililegeza kiasi vikwazo na kuruhusu msaada zaidi na bidhaa kuingia Gaza. Lakini Gunness anasema bado haitoshi, na UNRWA inahitaji kujenga shule 100 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, kujenga nyumba 10,000 na vituo vya afya sita, lakini hadi sasa Israel imeidhinisha miradi 43 tuu kati ya yote iliyowasilishwa na UNRWA.