Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu la UM lajadili hali ya Ivory Coast

Baraza la haki za binadamu la UM lajadili hali ya Ivory Coast

Kikao maalumu cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kimefanyika mjini Geneva leo kujadili hali ya haki za binadamu nchini Ivory Coast.

Naibu kamishna mkuu wa haki za binadamu Bi Kyung-wha-Kang ameliambia baraza hilo kwamba hali ya haki za binadamu nchini Ivory Coast inazidi kuwa mbaya, amesema namba maalumu ya simu iliyowekwa na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo kwa ajili ya kupata msaada inapokea simu zaidi ya 300 kwa siku za madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Bi Kang amesema katika wiki moja iliyopita watu 173 wameuawa, 471 kukamatwa na 24 hawajulikani waliko. Amelaani kitendo cha wafuasi wa bwana Laurent Gbagbo kutumia radio na televisheni ya taifa na magazeti mengine binafsi kuchochea chuki na ghasia miongoni mwa watu.

(SAUTI YA KYUNG-WHA-KANG)

Mswaada wa azimio uliowasilishwa kwenye baraza hilo umetoa wito kwa pande zote nchini Ivory Coast kukomesha ukiukaji wa haki za binadamu, kuheshimu matakwa ya watu, kurejesha demokrasia na utawala wa sheria.