Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi tajiri zinawaacha nyuma watoto:UNICEF

Nchi tajiri zinawaacha nyuma watoto:UNICEF

Ripoti iliyotolewa leo na kituo cha utafiti cha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imebaini kwamba watoto katika nchi nyingi tajairi za Ulaya na Marekani wanakabiliwa matatizo ya kutokuwepo na usawa ikilinganishwa na mataifa mengine yaliyoendelea.

Ripoti hiyo iliyoitwa "watoto wanaachwa nyuma" kwa mara ya kwanza inaziorodhesha nchi 24 zilizo na matatizo ya usawa katika masuala ya afya, elimu na mahitaji muhimu ya maisha kwa watoto. Ripoti hiyo imejikita katika suala moja nalo ni kutokuwepo usawa, na inahoji ni kwa kiasi gani nchi tajiri zinaruhusu watoto kuangukia katika tatizo hilo.

Italia, Marekani, Ugiriki, Ubelgiji na Uingereza kwa mfano imebainika kuruhusu watoto kuachwa nyuma ukilinganisha na nchi kama Denmark, Finland, Ireland, Switzerland na Uholanzi. Ripoti hiyo imeonya kwamba athari za watoto kuachwa nyuma ni kubwa pia katika uchumi na jamii kwa ujumla. Ripoti hiyo pia imepima tofauti kati ya watoto wanaochukuliwa kuwa ni wa maisha ya kawaida na wale masikini kabisa.