Ongezeko la wakimbizi wa ndani linatia hofu Afghanistan

Ongezeko la wakimbizi wa ndani linatia hofu Afghanistan

Wakati huohuo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linahofia ongezeko la wakimbizi wa ndani kutokana na machafuko nchini Afghanistan.

Shirika hilo linasema wasiwasi wao ni kwamba mara nyingi inakuwa ni hatari kubwa kuweza kuwasaidia. Kati ya Juni 2009 na Septemba 2010 watu 120,000 walilazimika kuzikimbia nyumba zao kwa sababu ya vita, ikiwa ni ongezeko la wakimbizi wa ndani 319,000 na idadi hiyo haijumuishi wakimbizi walioko katika maeneo ya viungani ambako kuwahesabu na kujua idadi yao ni tatizo. Jayson Nyakundi na taarifa zaidi.

(RIPOTI YA JAYSON NYAKUNDI)

Baadhi ya wakimbizi hawa wanaripotiwa kuhama makwao kutokana na majanga ya asili hususan mafuriko na pia mizozo ya ardhi. Wizara inayohusika na masuala ya wakimbizi nchini Afghanistan inakadiria wakimbizi wa ndani kufikia 500,000 wakati wengi wanapopatikana kwenye maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi yanayosemekana kutokuwa salama na yasiyofikiwa na wafanyakazi wa kutoa misaada.

Huku majira ya baridi yakikaribia UNHCR inasema kuwa ina mpango wa kusambaza nguo za kutoa joto, makaa na mablanketi kwa maelfu ya wakimbizi wa ndani wakati nalo shirika na mpango wa chakula duniani WFP likisema kuwa linashirikiana na UNHCR kuwasaidia wakimbizi hao.

Msemaji wa WFP Challiss McDonough anasema kuwa shirika hilo litatoa chakula kwa wakimbizi 320,000 wanaoishi katika hali mbaya.