Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imetaka kuwepo msaada kwa waomba hifadhi Ugiriki

UNHCR imetaka kuwepo msaada kwa waomba hifadhi Ugiriki

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeitaka jumuiya ya muungano wa Ulaya kuangalia upya namna inavyoweza kuwasaidia wakimbizi na waomba hifadhi wa Ugiriki.

Hatua hiyo imekuja baada ya timu ya maafisa wa muungano wa Ulaya inayoshughulikia mipaka FRONTEX kupelekwa Ugiriki kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kupambana na idadi kubwa ya wahamiaji wanaovuka mpaka na kuingia Ugiriki kila siku. George Njogopa na taarifa zaidi.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

UNHCR imesema kuwa inafahamu fika changamoto inayoibuka kwa Ugiriki lakini kwa kuzingatia hali ngumu wanayokumbanayo wakimbizi hao, lazima kutafakari upya hatua hiyo kwani inaweza kuwaathiri hata wale wanaomba hifadhi toka kwa jumuiya za kimataifa.

Karibu wahamiaji haramu tisa kati ya kumi wanaitumia Ugiriki kama njia ya kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya. Idadi ya watu wanaoingia katika nchi hizo kwa usafiri wa nchi kavu imeongezeka kwa zaidi ya theluthi kwa mwaka.