Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Global Fund kupata mabilioni kupambana na ukimwi, TB na malaria

Global Fund kupata mabilioni kupambana na ukimwi, TB na malaria

Wahisani waahidi mabilioni ya dola kusaidia Global Fund kupambana na Malaria, Kifua kikuu na ukimwi.

Nchi wahisani, wafadhili binafsi, mashirika na watu binafsi wamekutanika pamoja kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na kuahidi kitita kipya cha fedha kusaidia mfuko wa kimataifa Global Fund ili kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria.

Mratibu wa Marekani wa masuala ya kimataifa ya ukimwi Eric Goosby leo ametangaza kwamba Marekani chini ya utawala wa Rais Barack Obama na waziri wa mambo ya nje Hilary Clinton inaahidi kutoa dola bilioni 4 kusaidia Global fund kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria katika kipindi cha 2011 hadi 2013. Ahadi hiyo ndio kubwa kabisa kuwahi kutolewa na muhisani kwa mfuko wa kimataifa na ni mchango mkubwa kabisa wa muhisani mmoja utaowahi kutolewa kwa mfuko huo.

Marekani ni mchangiaji mkubwa wa Global Fund. Mkurugenzi mkuu wa Global Fund Michel Kazatchkine amesema kwa ahadi ya Marekani kwa miaka hiyo mitatu nchi hiyo imeonyesha kujidhatiti kwake katika juhudi za kimataifa kukabiliana na ukimwi, kifua kikuu na malaria. Ameongeza kuwa ahadi hiyo ya Marekani ni mfano wa kuigwa na wahisani wengine na wanaimani itakuwa chachu.

Juhudi za Global Fund zimesaidia kuokoa maisha ya watu takriban milioni 5.7 kwa kuwapa tiba ya HIV watu milioni 2.8 na kifua kikuu watu mulioni 7 , huku mfujko huo ukigawa vyandarua vya mbu milioni 122 kuzuia malaria. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameishukuru Global Fund na wahisani wote kwa kazi zao na ushiriki wao katika kuokoa maisha ya watu, na amesema msaada wa wahisani ukiongezeka maisha zaidi yatanusurika.

Ameongeza kuwa kwa juhudi hizo kwa pamoja tunaandika habari ya mafanikio ya kihistoria katika karne hii ya 21.  Amesema ahadi za fedha mnazotoa zinaokoa maisha ya mamilioni, na zaidi ya hapo zinatoa matumaini, kuwekeza kwa Global fund ni kuwekeza kwa maendeleo.

Global Fund ilianzishwa mwaka 2002 ili kuchagiza juhudi za kupambana na maradhi matatu yanayouwa mamilioni ya watu duniani, ukimwi, kifua kikuu na malaria, na kuzipekeka fedha kule zinakohitajika zaidi. Hadi hii leo Global Fund imeshatumia dola bilioni 19.3 kwa kusaidia nchi 144 kuzuia, kutibu na miradi ya kuwasaidia waathirika wa magonjwa hayo matatu.