Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waitaka Israel kuafiki urefushwaji muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi

UM waitaka Israel kuafiki urefushwaji muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi

Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wake juu ya masuala ya kidiplomasia wanaojishughulisha na utafutaji wa amani katika eneo la Mashariki ya Kati, wameitolea mwito Israel kurefusha muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi iliyokaliwa katika Ukingo wa Magharibi, ili kuruhusu kuendelea tena kwa mazungumzo yenye shabaya ya kutanzua mzozo huo.

Lakini pia wamezitaka nchi zilizopo kwenye mafungamano ya Kiarabu kuunga mkono mazungumzo hayo ambayo yalisimama wiki iliyopita baada ya pande hizo mbili Israel na Palestina kutofautiana juu ya suala hilo.

Ukiunga mkono kuanza kwa majadiliano ya ana kwa ana baada ya kipindi cha miezi 19, taarifa iliyotolewa kwa pamoja pande zinasimamia mazungumzo ya uletaji amani kwenye eneo hilo imetaka pande hizo kujenga hali ya kuaminiana ili kurahisha zoezi la utanzuaji wa mzozo huo.

Kundi hilo ambalo linajumuisha Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Russia na Marekani imerejea wito wake wa kuitaka Israel kutambua kuwa majadiliano hayo yaliyoanza upya yanaweza kuleta tija kama itazingatia suala la urefushwaji wa muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi hayo unaomalizika mwisho wa mwezi huu.