Naibu Katibu Mkuu wa UM akutana na Rais Sheikh Sharif Mogadishu
Naibu Katibu anaehusika na masuala ya kisiasa Lynn Pascoe ameeleza uungaji mkono wake na wananchi wa Somalia wakati wa ziara yake ya siku moja mjini Mogadishu siku ya Jumatano. Bw Pascoe aliyefuatana na mwakilishi maalumu wa UM huko Somalia Augustine Mahiga, alikutana na rais Sheikh Sharif na baraza lake la mawaziri katika ikulu ya Villa Somalia huko Mogadishu.
Bw Pascoe aliwahimiza viongozi wa serikali ya mpito TFG kujadiliana na makundi mengine na kuzingatia juu ya kuitawala nchi. Anasema ni muhimu sana kuwaonesha wananchi wa Somalia kwamba serikali inaweza kutoa huduma za msingi, na kwamba jumuia ya kimataifa ina hamu kubwa ya kuisaidia TFG . Lakini serikali yenyewe inahitaji kufanya kazi zaidi na kuweza kufanya kazi kwa ushirikiano.
Pascoe na Mahiga walikutana na mkuu wa kikosi cha amani cha Umoja wa Africa AMISOM pamoja na walinda amani wake na kutembelea hospitali ya AMISOM ambako walishuhudia walinda amani wakiwapatia matibabu raia wa Somalia. Naibu Katibu Mkuu yuko katika ziara ya eneo la Pembe ya Afrika katika lengo la kuhamasisha juhudi za amani na utulivu huko Somalia.