Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya UM juu ya ukiukaji wa haki za binadamu DRC itatolewa mwezi ujao

Ripoti ya UM juu ya ukiukaji wa haki za binadamu DRC itatolewa mwezi ujao

Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba ripoti inayo orodhesha ukiukaji mbaya kabisa ulotendwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya 1993 hadi 2003 itatolewa tarehe mosi Oktoba.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu OHCHR, inasema ripoti hiyo na matokeo ya uchunguzi wake itahusu vitendo vilivyotokea katika kipindi cha miaka kumi kote nchini DRC na wala si maeneo yaliyokumbwa na vita vya mashariki pekee yake.

Lengo kuu la ripoti ni kuwasaidia watu wa nchin hiyo kuunda mfumo wa mpito wa mahakama na kusaidia katika vita dhidi ya kutoadhibiwa watu. Ripoti hiyo iliyotolewa kwa siri na kuchapishwa na gazeti la kifaransa la Le Monde, inaeleza juu ya zaidi ya visa 600 vilivyotokea huko DRC mnamo kipindi cha miaka 10 ambapo maelfu na maelfu ya watu waliuwawa, na imetaja idadi fulani ya makundi yaliyohusika na ukiukaji huo.

Kamishna mkuu Navi Pillay anasema kufuatia ombui la serikali tumeamua kuipatia muda wa mwezi mmoja zaidi kutoa maoni yao juu ya rasimu ya ripoti. Anasema watachapisha maoni yeyote ya serikali pamoja na ripoti hiyo hapo Oktoba mosi ikiwa watapendelea kufanya hivyo. Zaidi ya mashahidi 1, 280 walihojiwa kutoa ushahidi au kulinganisha na tuhuma za ukiukaji zilizotolewa ikiwa ni pamoja na vitendo vya zamani ambavyo havikuorodheshwa.