Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waisaidia Cameroon baada ya kuzuka kipindupindu

UM waisaidia Cameroon baada ya kuzuka kipindupindu

Mashirika matano ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanapeleka msaada wa madawa na vitu vingine kwa Kaskazini mwa Cameroon ambako mlipuko wa kipindupindu umeshakatili maisha ya watu 155.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linasema limepeleka dawa kama oral rehydration salt, vifaa vya usafi, gloves, maji ya kunywa na vifaa vya elimu. UNICEF inasema inashirikiana na mshirika mengine kama UNFPA, WFP na UNHCR pamoja na wizara za serikali na shirika la msalaba mwekundu ili kufikisha msaada kwa maelfu ya watu hususan wanawake na watoto.

Ora Musu afisa wa UNICEF nchini Cameroon anasema eneo lililoathirika zaidi ni Kaskazini mwa nchi linalopakana na Nigeria, Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako ni makazi ya watu wapatao milioni 5 na wanakabiliwa na matatizo ya maji safi ya kunywa na usafi. Ameonya kuwa tangu kuzuka ugonjwa huo ni miezi mine sasa na kuna hofu ya uwezekano wa kusambaa na kuingia katika nchi jirani.