Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeitaka miji kuongoza vita dhidi ya maambukizi ya ukimwi

UM umeitaka miji kuongoza vita dhidi ya maambukizi ya ukimwi

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS ametoa wito kwa miji duniani kuwa msitari wa mbele kuufanya ukimwi kuwa historia kwa kuongeza juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo.

Michel Sidibe amesema wakati asilimia 70 ya watu wote duniani wnatarajiwa kuishi mijini ifikapo 2050 kila watu 7 kati ya 10 watakuwa wakazi wa mjini na kufanya kuwa na wakazi takribani milioni 10 katika kila mji.

Sidibe akizungumza na zaidi ya viongozi wa sekta ya afya na washiriki 100 mjini Shangai Uchina, amesema wakati ni bayana kwamba miji ni muhimu katika vita dhidi ya ukimwi, haijawezeshwa na kuhamasishwa vya kutosha kuchukua hatua.

Amesema kukua haraka kwa miji kumesababisha ongezeko la maambukizi ya HIV na inakadiriwa kwamba karibu asilimia 50 ya watu wanaoishi na virusi vya HIV wako mijini. Amesema na katika miji mingine kiwango cha maambukizi ni cha juu sana mfano kama Durban Afrika ya Kusini kuna watu 740,000 wanaoishi na HIV idadi ambayo ni sawa na wato wote wenye HIV nchini Uchina. Mkuu huyo wa UNAIDS ameonya kwamba endapo hali hiyo itapuuziwa basi maambukizi yataongezeka, umsikini utaongezeka, wasio na makazi watazidi na mfumo mzima wa jamii kuwa hatarini.