Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa Kenya leo wamepiga kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba

Wananchi wa Kenya leo wamepiga kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba

Wananchi wa Kenya leo wamepiga kura muhimu ya maoni kuamua hatma ya katiba mpya ya nchi hiyo, huku viongozi wakitoa wito wa kuwepo na amani kote nchini.

Kura hii ya maoni inafanyika miaka miwili baada ya mamia ya watu kuuawa katika ghasia zilizozuka punde baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Katiba mpya imelenga kubadilisha mfumo wa siasa za Kenya na kuzuia kutokea tena kwa ghasia hizo zilizosababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Kura ya maoni imeonyesha kuwa katiba hiyo itakubaliwa na wananchi. Wanaoiunga mkono katiba wanasema kuwa itachangia ugawanaji wa mamlaka kwa kuunda utawala wa majimbo, kumaliza ukabila na pia kusuluhisha au kuleta mabadiliko katika sera ya ardhi.

Miongoni mwa viongozi waliotoa wito wa amani wakati wa shughuli hiyo ni rais Mwai Kibaki, Waziri mkuu Raila Odinga na viongozi wa tume ya muda wa uchaguzi nchini humo, IIEC.