Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waonya juu ya ukiukaji wa haki kuelekea uchaguzi Burundi

UM waonya juu ya ukiukaji wa haki kuelekea uchaguzi Burundi

Burundi iko katika maandalizi ya mwishomwisho kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais unaotarajiwa kufanyika Jumatatu ijayo Juni 28.

Zikiwa zimesalia siku mbili tuu kabla ya uchaguzi huo mtaalamu wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa Akich Okola ametoa wito wa kuwepo na mazungumzo baina ya serikali na vyama vyote vya siasa ili kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa amani na wa kidemokrasia. Amesema katika ziara yake nchini humo alibaini kwa hofu kufuatia kuongezeka kwa taarifa za ukiukaji wa haki za binadamu na usalama, hasa wakati wa uchaguzi wa madiwani Mai 24 mwaka huu, ambapo idadi kubwa ya watu walikamatwa, wengine kuwekwa mahabusu, na wanasiasa na wafuasi wa upinzani kusumbuliwa.

Pia amesema aligundua kuwa hali ya usalama imezorota huku mashambulizi ya magruneti yakiarifiwa mara kwa mara. Ameongeza kuwa hofu yake ni kwamba hali hii itazidisha ukiukaji wa haki za binadamu na ghasia. Amevitolea wito vyama vyote vya siasa kuendelea kushiriki mchakato huo wa uchaguzi huo.