Skip to main content

Hali imeanza kuwa tulivu katika miji ya Kyrgystan asema afisa wa UM

Hali imeanza kuwa tulivu katika miji ya Kyrgystan asema afisa wa UM

Afisa wa Umoja wa Mataifa amesema wakati haki ya utulivu imerejea katika miji ya Kyrgyzstan ya Osh na Jalal-Abad , hofu ya mivutano ya kikabila na uvumi wa machafuko unazidi.

Mwakilishi msaidizi wa Katibu Mkuu katika masuala ya kisiasa Oscar Fernandez-Taranco, ameyasema hayo katika taarifa yake kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kuhusu hali ya Kyrgyzstan . Na Umoja wa Mataifa umesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa wakimbizi na waliosambaratishwa na machafuko ambao sasa wameanza kurejea nyumbani , na pia kuepuka chochote kinakachochagiza kuzuka tena kwa machafuko.

Mwakilishi huyo amepongeza juhudi za mashirika ya Umoja wa Mataifa kutoa misaada ya kibinadamu lakini amesema usalama mdogo unaendelea kukwamisha ugawaji wa misaada hiyo. Fernandez-Taranco ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unatoa msaada wa kiufundi kuusaidia uongozi wa tume ya uchaguzi ya Kyrygystan ambao umejidhatiti kuendesha kura ya maoni Juni 27 mwaka huu.