Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano baina ya nchi za Asia ya Kati na Afghanistan ni dhahiri- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama. PichaUM/Manuel Elias

Ushirikiano baina ya nchi za Asia ya Kati na Afghanistan ni dhahiri- Guterres

Umoja wa Mataifa umesema uko tayari kusaidia nchi za Asia ya Kati zinapoimarisha ushirikiano baina yao na Afghanistan ili kufanikisha malengo ya amani, maendeleo endelevu, utulivu na usalama.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amesema hayo leo wakati akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama uliokutana kujadili ubia wa kikanda kati ya Afghanistan na Asia ya Kati.

Bwana Guterres ametolea mfano ushirikiano wa kielimu uliopo sasa kati ya Kazakhstan na Afghanistan..

(Sauti ya António  Guterres)

“Zaidi ya wanafunzi 500 kutoka Afghanistan wamehitimu mafunzo ya vyuo vikuu na vile vya ufundi nchini Kazakhstan, na karibu wengine zaidi ya 500 wanahitimisha masomo yao. Kazakhstan imetenga dola milioni 50 kwa mpango huu. Uzbekistan nayo iko kwenye mwelekeo huo.”

Kama hiyo haitoshi ametaja Uzbekhstan ambayo nayo imezindua safari za moja kwa moja za ndege kutoka mji wake mkuu Tashkent hadi mji mkuu wa Afghanistan, Kabul bila kusahau miradi ya kuunganisha pande hizo kwa njia ya reli, akisema inachochea ukuaji mkubwa aw uchumi.

image
Watoto nchini Afghanistani wakiwa safarini kuelekea katika moja ya sherehe nchini humo. (Picha:UN/Fardin Waezi)
Hata hivyo ametaja jambo muhimu la kushughulikia kuwa ni hofu ya usalama nchini Afghanistan, akisema ndio hoja inayoshamiri katika uhusiano baina ya nchi za Asia ya Kati na Afghanistan, hivyo amesema.

(Sauti ya António  Guterres)

“Mkutano ujao wa Kabul kuhusu mchakato wa amani na ushirikiano wa kiuchumi utakuwa ni fursa kwa serikali ya Afghanistan kuweka dira yake makini kabisa kuhusu mchakato wa amani na usalama ukihusisha pia jitihada za kikanda za kutokomeza ugaidi na misimamo mikali. Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia.”