Skip to main content

KM awaambia wajumbe wa Mkutano juu ya Mfuko wa CERF "twahitajia misaada zaidi kukabili athari za gesi chafuzi"

KM awaambia wajumbe wa Mkutano juu ya Mfuko wa CERF "twahitajia misaada zaidi kukabili athari za gesi chafuzi"

Asubuhi kwenye Makao Makuu, kulifanyika kikao maalumu kuzingatia shughuli za ile Taasisi ya Mfuko wa UM juu ya Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF.

KM kwenye risala yake aliwaambia wajumbe wa kimataifa ya kuwa atakapohudhuria Mkutano wa Copenhagen juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, wiki ijayo, atatilia mkazo ule ukweli hakika uliothibitisha kwamba mageuzi ya hali ya hewa, kwa sasa hivi, yanaathiri zaidi, kila mwaka, mamilioni ya watu wanaoishi katika sehemu mbalimbali za dunia, mabadiliko ambayo huzusha mafuriko makuu ya mara kwa mara kwenye maeneo yao, yakichanganyika na dhoruba kali pamoja na ukame wa kihistoria. Wale wanaoumia zaidi na maafa haya, alikumbusha KM, huwa ni watu masikini waliokosa uwezo wa kumudu madhara yanayochohewa na hali hii. Alisema kutokana na mazingira haya chafuzi, mashirika ya kimataifa yenye kuhudumia misaada ya kiutu yatahitajia kufadhiliwa na wahisani wa kimataifa fedha zaidi kukidhi mahitaji ya waathirika wa majanga ya ukosefu wa chakula, na matatizo ya kung'olewa makazi, hatari za afya na masuala mengineyo yenye kuhatarisha maisha ya kawaida.