Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko wa Global Fund wanusuru maisha ya watu milioni 4.9 duniani

Mfuko wa Global Fund wanusuru maisha ya watu milioni 4.9 duniani

Mfuko wa Kimataifa Kupiga Vita UKIMWI, TB na Malaria (Global Fund) imetangaza leo hii, kutokea Geneva, matokeo ya shughuli zake za mwaka, katika kupambana na maradhi haya matatu.

Ripoti ya Taasisi ya Global Fund imeeleza, kutokana na mchango wake katika kusaidia miradi ya afya, katika nchi 140, watu milioni 2.5 wanaoishi na virusi vya UKIMWI ulimwenguni waliweza kupatiwa dawa za kurefusha maisha, wagonjwa milioni 6 walifanikiwa kutibiwa kifua kikuu (TB), miradi ambayo vile vile iliwezesha kufadhilia vyandarua milioni 104 vilivyonyunyiziwa dawa kinga ya kuzuia maambukizo ya malaria. Kadhia hii ilinusuru maisha ya watu milioni 4.9, fungu la umma wa kimataifa ambao bila ya kufadhiliwa msaada wa tiba kutoka Taasisi ya Global Fund wangelifariki, mchango wenye kuzuia vifo 3,600 kila siku kutukia ulimwenguni. Taasisi imeshatoa msaada wa fedha kwa miradi 500, unaogharamia dola bilioni 9.3, mchango unaojumlisha robo moja ya misaada yote ya kimataifa inayotumiwa kupambana na UKIMWI, na vile vile hujumlisha khumsi tatu (au sehemu tatu ya tano) ya misaada yote inayofadhiliwa kimataifa katika kudhibiti TB na malaria.