Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtetezi wa haki za watoto asema kasumbuliwa sana na ripoti za watoto wanaoshirikishwa na wapambanaji katika Sudan

Mtetezi wa haki za watoto asema kasumbuliwa sana na ripoti za watoto wanaoshirikishwa na wapambanaji katika Sudan

Radhika Coomaraswamy, Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Haki za Watoto Walionaswa kwenye Mapigano, ameripotiwa kuwa ana wasiwasi juu ya taarifa alizopokea, zinazoonyesha watoto walio chini ya umri wa utu uzima, wameruhusiwa kujiunga na makundi ya waasi wa katika Sudan.

Alisema alishtushwa pia na zile taarifa nyengine zenye kudai Vikosi vya Jeshi la Usalama vimegunduliwa kuwahusisha watoto wadogo kwenye shughuli za kijeshi. Coomaraswamy aliyasema haya baada ya kukamilisha ziara ya siku kumi nchini Sudan, ambapo alitembelea miji ya Khartoum, El Fasher na El Geneina katika Darfur, na pia kuzuru miji ya Juba, Yambio na Bor katika Sudan Kusini. Coomaraswamy vile vile alikaribisha utiaji sahihi wa tarehe 20 Novemba, uliofanyika kwenye mji wa Juba, wa ule mradi wa utendaji wa kundi la SPLA wa kukomesha utumiaji wa watoto kama wapiganaji. Halkadhalika, aliipongeza Serikali ya Muungano wa Taifa kwa maendeleo yao ya miaka miwili ambapo iliwapatia watoto ulinzi na hifadhi bora, na pia kuwapatia sauti ya kujieleza hadharani wale waathirika wa makosa ya udhalilishaji wa kiijinsia. Aliisihi Serikali kupitisha sheria ya dharura, ya kupambana na mabavu ya kunajisi kijinsia, kanuni ambazo zitajumlisha uzuiaji wa vitendo hivyo haramu na kuadhibu wale wanaokutikana na makosa haya ya jinai.