Fafanuzi fupi juu ya mkutano wa UNIFEM kwa wanawake wa Darfur Kaskazini
Mnamo wiki iliopita, wanawake 500 ziada, kutoka fani na kazi mbalimbali walikusanyika katika Chuo Kikuu cha El Fasher, Darfur Kaskazini kusailia amani na utulivu kwenye eneo lao, na taifa, kwa ujumla.
Wanawake kadha waliwasilisha maoni binafasi juu ya suala hilo, ikijumlisha wawakilishi wa makundi ya wanawake kutoka Sudan Kusini, ambao walisafiri masafa marefu kutokea mji wa Juba, na walielezea juu ya uzoefu unaoambatana na maendeleo ya wanawake kwa uwiano na wanawake wenzi wa jimbo la magharibi la Sudan la Darfur. Mkutano ulitayarishwa na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Wanawake (UNIFEM). Mshauri Mkuu wa UNIFEM juu ya Masuala ya Kijinsiya, Andrea Cullinan, ambaye alihudhuria mkutano, alinakiliwa akisema UM unaelewa vyema "matatizo wanayokabiliwa nayo wanawake wa Sudan ... na namna mapigano, ya kwenye maeneo yao, yalivyoathiri wanawake kushinda wanaume ... hasa ilivyokuwa ripoti zimethibitisha kihakika kwamba wanawake ndio fungu kubwa lenye kusumbuliwa zaidi na mapigano, na sasa hivi wanahitajia kupatiwa, haraka iwezekanavyo, suluhu ya kudumu juu ya vurugu dhidi yao." Aliongeza kwa kusema mkusanyiko wa wanawake wa kutoka maeneo yenye uhasama katika Sudan, uliofanyika kwenye Chuo Kikuu cha El Fasher, umesaidia kuwapatia mabibi fursa ya kujadiliana kipamoja juu ya taratibu za kuleta suluhu itakayowakilisha amani ya kudumu katika Darfur.