Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO imeanzisha mradi wa kuotesha aina mpya ya mpunga Uganda kuwasaidia wakulima waathirika wa mapigano

FAO imeanzisha mradi wa kuotesha aina mpya ya mpunga Uganda kuwasaidia wakulima waathirika wa mapigano

Ripoti ya Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) imeeleza kwamba wahamiaji wa ndani ya nchi milioni 1.5 waliohajiri makazi yao baada ya miaka 20 ya mapigano na vurugu katika Uganda kaskazini, wameonekana hivi sasa wanaanza kurejea makwao baada ya kuishi maisha ya wasiwasi kwa muda mrefu nje ya maeneo yao.

Kichocheo cha wahamiaji kuchukua hatua hii kinatokana na mradi uanosimamiwa na FAO, ikishirikiana na Serikali ya Uganda, mpango unaojulikana kama mradi wa NERICA. Mradi wa NERICA umeanzisha utaratibu wa kilimo cha aina ya mpunga ambao unavumulia ukame, na mavuno yake yanazidi yale ya mpunga wa kienyeji kwa asilimia 30, na huzalisha aina ya mchele wenye ladha tamu na wenye lishe bora. Kadhalika mpunga huu hupevuka miezi mitatu tu baada ya kuoteshwa pindi patapatikana mvua za majira ya kawaida, ikiwakilisha maendeleo ya kisasa katika kadhia za kilimo. Kwa mujibu wa FAO mradi huu wa NERICA unachangisha pakubwa katika kuimarisha maendeleo yanayosarifika, ambayo yataisaidia Uganda kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ya kupunguza hali duni kwa waathirika wa umaskini nchini humo, hususan miongoni mwa wakulima wadogo wadogo kwenye yale maeneo ya kaskazini yenye ardhi mbaya.