Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raisi wa BK anasema UM unahitajia marekibisho adhimu kikazi

Raisi wa BK anasema UM unahitajia marekibisho adhimu kikazi

Ijumatatu, wakati Baraza Kuu (BK) la UM lilipokamilisha kikao chake cha mwaka, cha 63, wajumbe wa kimataifa waliarifiwa kwenye hotuba yake ya kufunga kikao, ya Raisi wa Baraza, ya kuwa UM unahitajia kufanyiwa marekibisho ya dharura na mabadiliko ya jumla ili uweze kuendeleza shughuli zake kwa mafanikio.

Raisi wa Baraza Kuu, Miguel d'Escoto wa Nicaragua alisema kuna mambo mengi yanayohitajia marekibisho ndani ya kazi za UM, kwa taasisi hii ya kimataifa kustahiki hishima na imani ya kuridhisha kutoka walimwengu. Raisi d'Escoto aliyalaumu baadhi ya Mataifa Wanachama yanayojichukulia hukumu za kipekee kinyume na haki za kimataifa, na bila kukhofu kuadhibiwa, hatua ambayo aliifananisha na kile alichokiita "kanuni za msituni ambapo mwenye nguvu anataka apishwe bila kujali sheria". Alitoa mfano wa suala la WaFalastina, suala ambalo alisema limemvunja moyo kuona hadi hivi sasa Mataifa Wanachama yameshindwa kulipatia suluhu, hali ambayo d'Escoto, alitilia mkazo, kuwa ni kashfa kubwa kabisa yenye kusababisha huzuni na masikitiko makubwa ya kiutu kwa umma husika.