Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoruhusu wahamiaji waliokwama baharini kuingia nchini kwaharamisha sheria ya kimataifa, ameonya Pillay

Kutoruhusu wahamiaji waliokwama baharini kuingia nchini kwaharamisha sheria ya kimataifa, ameonya Pillay

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay kwenye hotuba aliotoa Ijumanne mbele ya wajumbe waliohudhuria kikao cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, aliwashtumu vikali wale wenye mamlaka pamoja na manahodha wa meli kadha wanaoharamisha sheria za kimataifa wanapowakatalia kuwachukua wale wahamiaji walioachwa kutangatanga baharini.

Pillay alisema "mara nyingi wenye madaraka hukataa kuruhusu wahamiaji hawa kuingia nchini mwao, na huwaacha wakabili taabu, shida na hatari kuu baharini, na mara nyengine hata hupatwa na vifo, hasa pale wanaporudishwa baharini au kwenye meli na vyombo vyengine kwa kufanywa kama vinyesi hatari vyenye sumu inayodhuru." Alisema wingi wa wahamiaji hawa majaaliwa yao huwa yameshaamuliwa na wenye mamlaka pale wanapojaribu kuvuka bahari za Mediterranean, Ghuba ya Aden, visiwa vya Karabiani, Bahari ya Hindi na kwenye maeneo mengineyo ya bahari kuu. Alisisitiza kwamba ni wajibu kwa wenye madaraka wote kuwahoji wahamiaji walionaswa baharini kwa kuwafanyia uchunguzi kutambua kama wanahajiri makwao kwa sababu ya makandamizo na mateso! Alisema kwamba mara nyingi wahamiaji, kwa ujumla, hata wale wanaohama makwao kwa kupitia mipaka ya nchi kavu, nao pia hukataliwa bila huruma kuvuka mipaka.