Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Siku ya Kimataifa Kuzuia Kujiua' yakumbukwa na UM

'Siku ya Kimataifa Kuzuia Kujiua' yakumbukwa na UM

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaihishimu tarehe ya leo, Septemba 10, kuwa ni ‘Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani\'. Katika siku hii mashirika ya kimataifa hujaribu kuamsha hisia za umma wa kimataifa juu ya tatizo hili, suala ambalo ni mwiko kujadiliwa hadharani na jamii kadha wa kadha za ulimwengu.

Taarifa za WHO zinasema ni muhimu kwa suala hili kuzingatiwa, kwa ukamilifu kwenye matabaka yote ya jamii, kuanzia watu binafsi, maofisa wenye kushika hatamu za serikali pamoja na, vile vile, watu waliopoteza jamaa na ndugu wapendwa katika aila zao. Ripoti ya WHO imekadiria kwamba watu milioni moja ulimwenguni hujiua kila mwaka - sawa na watu 3,000 wanaojiua kila siku, sawa pia na mtu mmoja anayejiua katika kila nukta 40. Kadhalika ripoti ilieleza takwimu za watu wanaojaribu kujiua zimezidi baina ya mara 10 hadi 20 ya takwimu za watu waliojiua.