Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya watoto wachanga duniani vyaendelea kuteremka, inaripoti UNICEF

Vifo vya watoto wachanga duniani vyaendelea kuteremka, inaripoti UNICEF

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limetangaza takwimu mpya zilizokusanywa na wataalamu kutoka mashirika ya UM, ikijumlisha WHO, UNICEF, Benki Kuu ya Dunia na Kitengo cha UM juu Idadi ya Watu, takwimu ambazo zilionyesha viwango vya vifo vya watoto wachanga duniani, chini ya umri wa miaka mitano, viliteremka kwa asilimia 28 katika mwaka 2008.

Kwa mujibu wa takwimu hizi, mnamo 1990, katika kila watoto 1,000 waliozaliwa, chini ya miaka mitano, 90 ya watoto hawa walifariki, idadi ambayo katika 2008 iliteremka na kufikia vifo 65 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa. Jumla ya vifo vya watoto wachanga ulimwenguni katika 2008 ilikadiriwa kuwa milioni 8.8, wakati katika 1990 vifo hivyo vilijumlisha watoto wachanga milioni 12.5. Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Ann Veneman amesema kwamba licha ya kuwa tumeshuhudia maendeleo kwenye kadhia za kupunguza vifo vya watoto wachanga ulimwenguni, hasa katika miaka ya karibuni, hata hivyo jumuiya ya kimataifa hairidhiki hata kidogo na ile hali ambayo watoto wachanga milioni 8.8 bado wanaendelea kufariki kila mwaka kabla hawajatimia umri wa miaka mitano.