Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNICEF, mchezaji wa mpira wa kikapu washiriki kwenye ufunguzi wa taasisi za matibabu ya UKIMWI katika JKK

Mkuu wa UNICEF, mchezaji wa mpira wa kikapu washiriki kwenye ufunguzi wa taasisi za matibabu ya UKIMWI katika JKK

Ijumatano, kwenye mji wa Kinshasa, katika JKK kulifunguliwa rasmi maabara mbili muhimu za kufanyia uchunguzi wa kisayansi kuhusu kinga ya maradhi pamoja na usalama wa kazini kwa wahudumia afya ambazo zitakuwepo katika Hospitali ya kisasa ya Biamba Marie Mutombo (BMMH) iliojengwa na mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu kutoka JKK, Dikembe Mutombo.

Kadhalika taasisi hizi za Utafiti zilisaidiwa kifedha vile vile na Mungano wa Kampuni ya Becton, Dickinson (BD) ambayo inahusika na teknolojiya ya kupima afya. Taasisi inayohusika na usalama wa wahudumia afya inataraji kuwapatia mafunzo watumishi wa hospitali 300 ziada, wakati maabara mapya yaliojengwa kwa sasa yatatumiwa kuimarisha ufuatiliaji na matibabu ya wagonjwa wenye kuishi na VVU/UKIMWI. Ann Veneman, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), ambaye anazuru JKK sasa hivi, alikuwa miongoni mwa watu walioshiriki kwenye ufunguzi wa vituo vya uchunguzi katika hospitali ya BMMH. Alikumbusha kwenye hotuba alioitoa kwenye taadhima hizo ya kwamba "JKK ni mojawapo ya nchi maskini katika bara la Afrika, taifa ambalo kwa sababu ya kuelemewa na matatizo ya ufukara, mizozo na maradhi huchangisha katika kupalilia mizozo ya afya ya jamii kwa ule umma ulio dhaifu kihali." Alisema ushirikiano wa mashirika ya kimataifa na taasisi za afya katika JKK, kama ilivyoshuhudiwa kwenye mradi mpya wa hospitali ya BMMH, ni huduma ambazo anaamini zitasaidia sana katika kuyakabili matatizo ya afya yanayoangamiza umma dhaifu, na kuandaa miundombinu itakayopanua utunzaji wa afya na kuhudumia zaidi wale raia waliokosa uwezo wa kutumia vifaa kama hivyo kunusuru maisha.