Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la awali la atomiki Hiroshima lakumbukwa na Mkutano wa Kuondosha Silaha Duniani

Shambulio la awali la atomiki Hiroshima lakumbukwa na Mkutano wa Kuondosha Silaha Duniani

Tarehe ya leo, Agosti 06, 2009 ni siku ya ukumbusho wa kutupwa kwa bomu la kwanza la atomiki, na vikosi vya anga vya Marekani, katika mji wa Hiroshima, Ujapani miaka sitini na nne iliopita.

Mkutano wa Kuondosha Silaha Ulimwenguni, unaokutana hivi sasa mjini Geneva, uliandaa kikao maalumu juu ya kukumbukumbu hiyo. Balozi Caroline Millar wa Australia, Raisi wa Mkutano, kwenye risala yake alikumbusha kwamba tukio la Hiroshima limebainisha wazi kabisa, kwa walimwengu, maangamizi na uharibifu unaoletwa na silaha za kinyuklia, tukio ambalo pia linaonyesha umuhimu wa mataifa kurudia haraka majadiliano yao ili walimwengu wawe huru na silaha angamizi hizo, na vile vile kuhakikisha silaha za kinyuklia zitaondolewa kabisa duniani. Mwakilishi wa Ujapani, Akio Suda, ambaye taifa lake ndio lilioathirika na bomu la kwanza la atomiki, alisema kwenye risala yake kwamba siku ya leo, ikijumuika na tarehe 09 Agosti, ambapo bomu la pili la atomiki liliangushwa kwenye mji mwengine wa Ujapani wa Nagasaki, ni siku za umma wa kimataifa kukumbushana tena, ya kuwa wakati umewadia kwa Mataifa Wanachama kuongeza juhudi ziada ili kufikia mapema lile lengo adhimu la kuwa na ulimwengu ulioepukana milele na silaha za kinyuklia. Alisema Ujapani imeingiwa moyo kuona wajumbe wa kimataifa wamesisitiza kwenye risala zao kadha juu ya umuhimu wa kulitekeleza lengo hilo kipamoja. Kwa kuambatana na mwelekeo huo, Balozi wa Marekani Garold Larson alitangaza kwenye kikao cha kumbukumbu ya miaka sitini na nne ya kuangushwa kwa bomu la atomiki katika mji wa Hiroshima, ya kuwa mnamo mwezi Septemba Raisi wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kuongoza mkutano maalumu, wa kiwango cha juu katika Baraza la Usalama, kuzingataia masuala ya kuzuia uenezaji wa silaha za kinyuklia ulimwenguni na kudumisha ufyekaji wa silaha hizo kimataifa.