Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kuzuru Asia KM awaonya walimwengu juu ya hatari ya taathira za mabadiliko ya hali ya hewa

Baada ya kuzuru Asia KM awaonya walimwengu juu ya hatari ya taathira za mabadiliko ya hali ya hewa

Ijumatano, tarehe 29 Julai 2009, KM Ban Ki-moon alikuwa na mazungumzo na waandishi habari wa kimataifa waliopoMakao Makuu kuzingatia safari ya wiki moja aliyoyatembelea mataifa mawili ya Asia, yaani Uchina na Mongolia.

Alibainisha kwamba lengo hasa la safari yake hiyo ilikuwa ni kuangaza zile juhudi za kudhibiti bora taathira za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni, kama anavyoeleza hapa:

"Awali, nilitaka kuangaza jukumu muhimu la nchi kama

Uchina, katika kupiga vita kimataifa athari za mabadiliko ya 

hali ya hewa, na vile vile kuangaza mchango wa Uchina katika  kadhia hii."

Wakati KM alipokuwepo Uchina alishiriki kwenye taadhima ya kuanzisha mradi wa kutumia aina ya balbu za taa zenye kuhifadhi nishati, mradi ambao matumizi yake yataiwezesha Uchina kupunguza gharama za nishati kwa asilimia nane. Vile vile KM alipozuru Mongolia, baada ya Uchina, alipata fursa ya kujadiliana na wachungaji wanyama kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye maneo yao, ambapo robo tatu ya mbuga za malisho zinahatarishwa na kuenea kwa jangwa. KM alitupatia fafanuzi ifuatayo juu ya mkutano wake na wachungaji wa Mongolia:

"Mkutano wangu na jamii ya wachungaji nilioonana nawo kwenye mbuga wazi za Mongolia, ulinipatia fursa ya kushuhudia, kibinafsi namna wachungaji hawa wanavyohangaika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa kwenye mazingira yao, wakati wakijaribu kutafuta suluhu inayoridhisha kukomesha uharibifu huo. Wanajitahidi kubadilisha mazoezi ya matumizi yao ya ardhi, na wameanza hata kutumia nishatijua kuyatekeleza hayo. Wachungaji wa Mongolia wanajaribu kujirekibisha kwenye shughuli zao kwa kutumia utaratibu mpya, unaolingana na mapendekezo ya kimataifa ya kudhibiti bora taathira za mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini juu ya juhudi hizo, kwa sababu Mongolia ni taifa masikini, bila shaka linahitajia kusaidiwa kifedha na jumuiya ya kimataifa kwa wao kukamilisha huduma za kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa kwenye maeneo yao."

Katika nchi zote mbili za Asia alizozuru KM, yaani Uchina na Mongolia, wakati alipokuwepo huko, alitilia mkazo umuhimu wa Mataifa Wanachama kufikia maafikiano ya kuridhisha kwenye Mkutano Mkuu ujao wa Kudhibiti Taathira za Mabadiliko ya Hali ya Hewa Ulimwenguni, utakaofanyika mwezi Disemba mjini Copenhagen, Denmark. Kama inavyofahamika suala la mabadiliko ya hali ya hewa hupewa umuhimu wa hali ya juu na KM, na ndio maana kila anapozuru nchi wanachama, hachoki kukumbusha, mara kwa mara, juu ya taathira zake kwa ulimwengu mzima. Kwa kuambatana na mwelekeo huu, KM alitangaza kwamba mnamo siku za karibuni anatarajia kusafiri tena, kuelekea sehemu ya Ncha ya Kaskazini ya dunia (North Pole), ili kushuhudia, binafsi, namna athari za hali ya hewa zinavyochochea majabali ya barafu kuyayuka kwa kasi, hali ambayo husababisha kina cha bahari kupanda na kukithiri, na kuhatarisha yale mataifa yaliozungukwa na bahari, ambayo huenda yakaangamizwa na hali hii. Vile vile KM alikumbusha tena, kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo, majengo ya Makao Makuu ya UM, yaliopo kwenye jiji la New York, nayo pia yatafanyiwa marekibisho ya hali ya juu, yenye uwiano na sera mpya za kimataifa za kudhibiti taathira za mabadiliko ya hali ya hewa duniani, marekibishio ambayo yataisaidia taasisi yetu ya kimataifa kutumia nishati kwa ufanisi mkubwa zaidi, na kupunguza gharama ya nishati kwa asilimia 50, hali ambayo vile vile itapunguza umwagaji wa hewa chafu angani kutokana na shughuli za Makao Makuu kwa asilimia arobaini na tano.

Nikiripoti kutoka Makao Makuu ni AWK, Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya UM, NY.