Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za binadamu na jamii zinajadiliwa kwenye kikao cha ECOSOC

Haki za binadamu na jamii zinajadiliwa kwenye kikao cha ECOSOC

Halmashauri ya UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) inayokutana Geneva Alkhamisi ilizingatia masuala yanayohusu haki za binadamu na haki za kijamii, zenye kuambatana na huduma za maendeleo, uzuiaji wa uhalifu na mifumo ya sheria.

Sevil Atasoy, Raisi wa Bodi la Kimataifa juu ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya alisema kwenye taarifa yake kama walimwengu tunawajibika kukiri kihakika kwamba huduma za pamoja za kupambana na madawa haribifu dhidi ya jamii ni moja ya kadhia ilioleta mafanikio makubwa ya kimataifa katika karne ya ishirini. Alikumbusha kwamba asilimia 95 ya Mataifa Wanachama wa UM, yanayojumlisha asilimia 90 ya idadi ya watu duniani, yameridhia na kuidhinisha vifungu vya mikataba inayohusu udhibiti bora wa madawa haramu ya kulevya, maafikiano ambayo yamesaidia kwenye zile shughuli za kuzuia uenezaji wa madawa hayo ya kulevya duniani, licha ya kuwa idadi ya watu wanaotamani sana kutumia madawa haya nayo vile vile inazidi kukithiri.