Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za dharura zahitajika kupunguza shida za ajira kwa wafanyakazi wahamaji waliopo nje, inasihi UNCTAD

Hatua za dharura zahitajika kupunguza shida za ajira kwa wafanyakazi wahamaji waliopo nje, inasihi UNCTAD

Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, (UNCTAD) limearifu kwamba muongezeko wa ukosefu wa kazi ulimwenguni kwa sababu ya kuzorota kwa shughuli za kiuchumi katika soko la kimataifa, ni hali inayosababisha fungu kubwa la wafanyakazi waliohamia nchi za nje kuamua kurudi makwao.

Taarifa hii ilitangazwa kwenye kikao cha siku moja, cha ngazi ya juu, kinachofanyika Geneva Alkhamisi kuzingatia masuala ya wafanyakazi wahamaji na maendeleo ya uchumi, katika kipindi ambacho ulimwengu unakabiliwa na migogoro ya kifedha. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UNCTAD, Supachai Panitchpakdi, kwenye hotuba yake ya ufunguzi, aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano ya kuwa "mzozo wa fedha wa kimataifa huathiri sana shughuli za ajira kwa wafanyakazi wahamaji", wafanyakazi ambao malipo yao wanaotuma makwao mara nyingi husaidia kufufua uchumi wa nchi zao. Mkuu wa UNCTAD aliashiria ukosefu wa kazi utaendelea kuselelea kwa mwaka huu, ambapo katika mwisho wa 2009, idadi ya watu wasioajiriwa kazi inakadiriwa kufikia watu milioni 60, takwimu ambayo humaanisha jumla ya watu wasiokuwa na kazi kimataifa kwa sababu ya mzoroto wa uchumi ulimwenguni itakuwa sawa na watu milioni 240.