Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICRC inasema miezi sita baada ya mashambulio ya Israel Ghaza inaendelea kusumbuka na kuteseka kimaisha

ICRC inasema miezi sita baada ya mashambulio ya Israel Ghaza inaendelea kusumbuka na kuteseka kimaisha

Ripoti mpya ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (ICRC) iliotangazwa hii leo, inaeleza ya kuwa umma wa eneo liliokaliwa la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza, unaendelea kusumbuka na kuteseka kimaisha, miezi sita baada ya operesheni za kijeshi za Israel kuendelezwa dhidi ya eneo hili la Mashariki ya Kati.

Ripoti ilisema watu wanaishi kwenye mazingira ambayo huwanyima uwezo wa kujihudumia kimaisha, na wanaendelea kuzama zaidi kwenye hali ya kukata tamaa kimaisha ambapo wakazi wa Ghaza hulazimika kubana matumizi, na wale walio wagonjwa sana huwa hawaruhusiwi hata kuondoka kwenda nje ya eneo kupata matibabu. Kadhalika, ripoti ya ICRC imethibitisha maelfu ya wakazi wa Ghaza, ambao nyumba zao ziliharibiwa na kuangamizwa na mashambulio ya Israel miezi michache iliopita, bado hawana makazi yanayofaa na wanaendelea kuishi kwenye majengo yaliobomolewa na yenye kuhitajia ujenzi mpya.