Skip to main content

Taarifa ya saba ya WHO kuhusu homa ya A/H1N1

Taarifa ya saba ya WHO kuhusu homa ya A/H1N1

Mnamo tarehe 30 Aprili, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mabadiliko kuhusu jina la vimelea vilivyozusha mgogoro wa homa mpya ya mafua. Kwa muda wa zaidi ya wiki, homa hii ilikuwa ikijulikana kama homa ya mafua ya nguruwe. Lakini hivi sasa jina rasmi la vimelea vya homa vitajulikana kama virusi vya homa ya mafua ya A/H1N1.

Taarifa ya WHO kuhusu mazingira ya maambukizo ya homa yalivyo ulimwenguni, kuanzia saa 06:00 kwa majira ya GMT, tarehe mosi Mei 2009 ni kama ifuatavyo: nchi 11 zimeripoti rasmi kugundua jumla ya wagonjwa 331 walioambukizwa na homa ya mafua ya H1N1 kwenye maeneo yao. Serikali ya Marekani imeripoti maabara zao za uchunguzi zimethibitisha watu 109 waliambukizwa na homa hiyo, ikijumlisha kifo cha mtoto mmoja. Mexico imeyakinisha tafiti za maabara zao zimethibitisha watu 156 waliambukizwa na homa ya mafua ya H1N1, na kusababisha vifo vya wagonjwa tisa. Kadhalika nchi nyengine tisa pia zimethibitisha kugundua wagonjwa waliopatwa na homa, nchi zenyewe ni Austria ambayo ilisajili mgonjwa mmoja wa homa ya mafua ya H1N1, Kanada imeripoti wagonjwa 34, Ujerumani watatu, Israel wawili, New Zealand wagonjwa watatu, Uholanzi mgonjwa mmoja, Uspeni 13, Uswiss mgonjwa mmoja na Uingereza imeripoti kuthibitisha watu wanane waliambukizwa na homa ya mafua ya vimelea vya aina ya A/H1N1.

Shirika la Afya Dunaini (WHO) vile vile limetoa taarifa inayoyanasihi Mataifa Wanachama kutotekeleza sera ya kupiga marufuku watu kusafiri au kufunga mipaka yao; na taarifa pia imependekeza kwa watu walio wagonjwa kujaribu kuchelewesha safari mpaka watakapojihisi wamepona, na wale waliojikuta na maradhi, baada ya safari za karibuni, walitakiwa kuhakikisha wanakwenda kuonana na daktari haraka iwezekanavyo, kwa kufuatana na mwongozo wa sekta ya afya za kizalendo. Kadhalika WHO imewahadharisha wale watu wanaokula nguruwe, kwamba uchunguzi wa maabara ya kimataifa umethibitisha kwamba hakujakutikana dalili zozote hatari zenye kuonyesha virusi vya homa vimeathiri nguruwe, na imewahimiza walaji nguruwe kuhakikisha wanapopika nyama huwa wanatumia halijoto kali. Halkadhalika watu wanatakiwa waoshe mikono, mara kwa mara, kwa kutumia maji safi na sabuni, na pia kuonana haraka na daktari, pindi wakihisi wamepatwa na homa ya mafua.