Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wabuni sera za kimataifa wahimizwa na FAO kuwashirikisha wakulima kwenye mijadala ya Mkataba wa Kyoto

Wabuni sera za kimataifa wahimizwa na FAO kuwashirikisha wakulima kwenye mijadala ya Mkataba wa Kyoto

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limetoa taarifa yenye kuwahimiza wabuni sera za kimataifa kuhusu udhibiti wa athari za mabadiliko ya hali hewa duniani kujumuisha suala la kilimo pale wanapozingatia mkataba mpya utakaofuatia Mkataba wa 1997 wa Kyoto, baada ya kukamilisha muda wake.

Alexander Muller, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa FAO aliwakumbusha wajumbe wanaohudhuria majadiliano ya UM yanayoendelea hivi sasa mjini Bonn kuhusu maafikiano yajayo ya kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa ya kwamba "ardhi ya kilimo imejaaliwa uwezo mkubwa wa kutenga, na kuzindika bora, hewa chafu". Kwa hivyo, alisisitiza juu ya umuhimu wa kuwashirikisha wakulima, hasa wale wanaoishi katika nchi maskini, kupata maoni yao, pale panapojadiliwa zile sera za kudhibiti bora, kimataifa, athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. UM umekadiria kilimo hujumlisha asilimia 14 ya umwagaji wa hewa chafu angani, na asilimia 17 nyengine hutokana na uchafuzi wa ardhi, kama zile shughuli za uchafuzi wa misistu.