Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UM yaonya athari kubwa Darfur baada ya kufukuzwa mashirika ya misaada

Mashirika ya UM yaonya athari kubwa Darfur baada ya kufukuzwa mashirika ya misaada

Mashirika ya huduma za dharura za UM yaongeza sauti zao za upinzani kufuatia onyo la KM Ban Ki-moon, na mashirika mengine ya UM kutokana na uwamuzi wa kuyafukuza mashirika 13 ya misaada kutoka Sudan.

Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, shirika la Afya Duniani WHO na Idara ya Huduma za Dharura OCHA, na Kamisheni ya Haki za Binadam, zimeeleza kwamba kiasi ya wa-Sudan milioni 4.7 - wakiwemo milioni 2.7 walokimbia makazi yao wanaopokea msaada wa dharura upande wa chakula, afya na maji, watakabiliwa na matatizo makubwa na kuna uwezekano wa kushuhudia idadi kubwa ya watu wakihama kutafuta maji na chakula. WHO inasema kuondoshwa kwa makundi yanayotoa huduma za afya kunaweza kupelekea kuongezeka idadi ya vifo, kupunguka huduma za chanjo na kuongezeka utapiamlo miongoni mwa watoto. OCHA inaeleza kwamba kufukuzwa kwa makundi hayo yasiyo ya kiserekali yanahatarisha operesheni yake kubwa kabisa duniani ya huduma za dharura, ambapo kwa mwake huu pekee UM umetoa mwito wa msaada wa dola bilioni 2.18.